Facebook yatengeneza toleo lingine la Messenger kwa ajili ya watoto

1286
Messenger Kids

Facebook imetangaza rasmi kuachiwa kwa toleo lingine la app ya Messenger ambayo limeundwa kwa dhumuni la matumizi ya watoto.

Toleo hilo jipya la Messenger limepewa jina la Messenger Kids na limetengenezwa maalumu kwa watoto wenye umri kuanzia miaka 6 mpaka 12.

Tofauti na Messenger ya kawaida, Messenger Kids haitohitaji mtoto kuwa na akaunti ya Facebook kutokana taratibu za kisheria ambazo haziruhusu matumizi ya mtandao huo wa kijamii kwa watu wenye umri chini ya miaka 13.

SOMA PIA: Facebook Messenger yaungana na PayPal kuwezesha ufanyaji malipo

Wazazi ndio watakuwa na wajibu wa kusimamia Messenger Kids za watoto wao kupitia akaunti zao za Facebook, ikihusisha kudhibiti marafiki ambao watoto wao wanaweza kuchati nao.

Pale ambapo mtoto atataka kuchati na rafiki yake, mzazi wa mtoto atahitaji kuwa na urafiki wa Facebook na mzazi wa rafiki huyo na kisha wazazi hao kutoka pande hizo mbili watatakiwa kuridhia watoto wao kuwasiliana kupitia app hiyo.

Facebook wamesema watatoa uangalizi mkubwa kwenye app hiyo na pia wameweka wazi kuwa app haitakuwa na matangazo yoyote na wala taarifa za watoto kutumika katika matangazo yoyote.