Tigo Tanzania na Uber waungana kuleta ofa mpya kwa wateja wao

531
tigo waungana na uber

Kampuni ya mtandao wa simu nchini, Tigo Tanzania imeingia katika makubaliano ya kipekee na kampuni ya teknolojia ya Uber. Kuanzia tarehe 19 Machi 2018, wateja wote wa Tigo wataweza kutumia huduma za app ya Uber bure! Makubaliano haya ya aina yake yatawafaidisha watumiaji wa huduma za usafiri za Uber pamoja na madereva waliojiunga na mfumo huo.

“Tigo ni nembo pana ya biashara katika soko la Tanzania na tuna wajibu wa kuzindua njia bora zaidi kwa wateja kujumuika katika maisha yanayowazingira. Makubaliano haya na Uber yanaboresha bidhaa na huduma ambazo wateja wetu wanafurahia katika maisha yao ya kila siku,” Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari alisema.

Naye Alfred Msemo, Mkurugenzi wa Uber alisema, “Tunafurahia makubaliano haya na Tigo yatakayowawezesha watumiaji na madereva wa huduma za Uber waliojisajili na mtandao wa Tigo kutumia huduma ya Uber App bure kwenye simu zao za mkononi bila tozo lolote la gharama za data. Uber ni mfumo wa simu za kisasa unaowezesha watu kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kubonyeza kitufe tu! Lengo kuu la Uber ni kuwezesha usafiri salama, wa uhakika na kwa gharama nafuu kwa kila mtu, kila sehemu. Makubaliano haya yatawahamasisha maelfu ya wakaazi wa Dar es Salaam ambao wamejisajili na mtandao wa Tigo kutumia Uber App kwa ajili ya huduma za usafiri jijini Dar es Salaam,’ Msemo alibainisha.

SOMA PIA: TTCL yazindua huduma mpya ya internet kwa matumizi ya nyumbani

Kampuni hizi mbili zitashirikiana katika bidhaa na promosheni zitakazoboresha huduma kwa wateja wa sasa na wa siku zijazo. Tigo na Uber nchini Tanzania wanatarajia kutangaza ofa zaidi kabambe zitakazowawezesha wateja kufurahia huduma za Uber jijini Dar es Salaam ambapo huduma za Uber zinapatikana kwa sasa.

Nini maoni yako kuhusu muungano huu, tuambie hapo chini.