VAR: Fahamu kuhusu mfumo mpya wa FIFA unaotumika Kombe la Dunia

295
VAR

VAR ni nini, sheria zake ni zipi, na unatumikaje katika michuano ya Kombe la Dunia inayofanyika huko Russia mwaka huu?

VAR ama ‘Video Assistant Referee’ ni mfumo mpya wa kwanza wa kiteknolojia katika mchezo wa mpira wa miguu unaotumia video ili kufanya maamuzi sahihi katika mchezo huo.

Mfumo huu ulianza kufanyiwa majaribio Uingereza katika kombe la FA na Carabao msimu uliopita, pamoja na ligi zingine mbalimbali katika nchi za Ujerumani na Italia.

Teknolojia hiyo imeanza kutumika rasmi mwaka huu katika mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea huko nchini Russia.

Si jambo la kushangaza kusikia teknolojia hiyo imezua mzozo kwa wapenzi wa mpira wa miguu lakini mpaka sasa imeonekana kusaidia kutatua matatizo mengi ya maamuzi ya uwanjani ambayo zamani yalikosa kupewa suluhisho na kuzua utata na ubishani miongoni mwa wapenzi wa mchezo huo.

SOMA PIA: Mwanafunzi Kenya aunda gari la nishati ya umeme wa jua

Kuhusu ufanyaji wa maamuzi uwanjani

VAR ni mfumo wa kiteknolojia unaopaswa kuwasaidia waamuzi wa uwanjani (refa na washika vibendera) kufanya maamuzi yaliyo sahihi ambayo wao hawakuweza kuyaona.

Maamuzi yanayofanywa na kupitia mfumo huo hufanywa na waamuzi wa nje ya uwanja ambao kazi yao ni kuangalia marudio ya matukio mbalimbali na kufanya mawasiliano na waamuzi wa ndani.

VAR inapaswa kutoa msaada kwa mwamuzi wa ndani katika maeneo makuu manne: magoli, penati, kadi nyekundu pamoja na maamuzi yaliyokosewa. Licha ya yote, bado mwamuzi wa ndani huwa anakuwa na msimamo wa mwisho katika ufanyaji maamuzi.

Magoli

Inapokuja suala la magoli mfumo huo hutumika sana katika matukio ya kuotea (offside), faulo zinazochezwa kabla ya goli kuingia, pamoja na masuala ya mpira kuvuka mstari.

Penati

VAR hugundua faulo zote zinazochezwa ndani ya eneo la goli na kumsaidia mwamuzi wa ndani kufanya maamuzi sahihi.

Kadi Nyekundu

Teknolojia hii huweka wazi rafu mbaya zinazochezwa na wachezaji ambazo zinahitaji adhabu ya kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Maamuzi Yaliyokosewa

Hapa hutumika pale mwamuzi wa ndani anapofanya maamuzi yasiyo sahihi, hivyo kuamua maamuzi kubadilishwa pale inapogundulika.

Je, nini maoni yako kuhusu mfumo wa VAR…?